*MAMA KIKWETE AWATAKA WATANZANIA KUTUMIA MAKTABA KUJISOMEA
Na Anna Nkinda – Maelezo
Watanzania
wametakiwa kutumia maktaba zilizopo kusoma vitabu na machapisho
yaliyopo ili waweze kujiongezea elimu na ufahamu zaidi wa masuala
mbalimbali yahusuyo maisha na elimu kwa upana wake.
Wito
huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akifungua
maktaba ya watoto iliyojengwa na Serikali ya Korea Kusini kupitia
Taasisi ya Step katika shule ya msingi Mzimuni iliyopo wilaya ya
Kinondoni jijinii Dar Es Salaam.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) alisema elimu ni ufunguo wa maisha na kwa njia hiyo Taifa
linaweza kupambana na kushinda vita dhidi ya maadui wakubwa watatu ambao
ni ujinga, umaskini na maradhi na matokeo ya ushindani huo ni
kupatikana kwa maendeleo.
“Pamoja
na mafunzo tunayoyapata shuleni, vyuoni na sehemu za kazi bado
tunapaswa kuendelea kusoma zaidi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya
kupambana na adui ujinga, maradhi na umaskini”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti
huyo wa Wama pia aliwataka walimu wa shule hiyo kutunza maktaba hiyo
ili iweze kukidhi malengo ya kuanzishwa kwake kwa kuandaa taratibu bora
za kusimamia matumizi na kuzuia upotevu na uharibifi wa vitabu na vifaa
vingine.
Kuhusu
suala la utandawazi Mama Kikwete alisema ni muhimu jamii ikatunza na
kuimarisha utamaduni ili hali wamo katika utandawazi kwani hivi sasa
Dunia imekuwa kama kiganja cha mkono kutokana na kukua kwa Sayansi ya
Teknolojia ila hayo yote yanawezekana ikiwa watasoma zaidi eneo husika
kulingana na mabadiliko yaliyopo.
Mama
Kikwete alisema, “Leo hii tumepata maendeleo kwa ajili ya Sayansi na
Teknolojia kwani ukitaka kujua chochote kinachoendelea Duniani ni rahisi
kwa kuwa unaingia katika mitandao na kuona, hili ni jambo zuri lakini
liendane na mila na utamaduni wetu siyo kila jambo unalichukua, chukua
yale mazuri ambayo yatakusaidia na yale mabaya ambayo hayana maslahi kwa
taifa yaache”.
Kwa
upande wake Balozi Young –Shim Dho ambaye ni Mwanzilishi wa Taasisi ya
Step na Balozi wa mradi wa Utalii endelevu kwa ajili ya kuondoa
umaskini wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani alimshukuru
Mama Kikwete kwa kuifungua maktaba hiyo na kuwataka wanafunzi kuitumia
kwa kujisomea.
Balozi
Young –Shim Dho alisema miaka michache iliyopita nchi ya Korea Kusini
ilikuwa ni moja ya nchi maskini Duniani lakini kupitia tabia ya kupenda
kusoma vitabu wamefanikiwa kuwa miongoni mwa nchi zilizomo ndani ya G20
na kuwataka watanzania kutumia vitabu hivyo kusoma.
“Kujengwa
kwa maktaba hii na zingine 23 na kupatikana kwa vitabu pamoja na vifaa
vingine vya maktaba ni jitihada za Mama Kikwete ambaye alizunguka huku
na kule kuomba msaada ambao leo hii umefanikiwa na kuweza kuwasaidia
watanzania wengi”, alisema Balozi Young –Shim Dho.
Ndani
ya eneo la shule ya Msingi Mzimuni kuna shule ya Msingi Mikumi ambapo
Mama Kikwete alimuomba balozi Young –Shim Dho kujenga maktaba kama hiyo
kwa ajili ya shule hiyo na Balozi huyo alikubali na kusema kuwa ifikapo
mwakani maktaba hiyo itakuwa imekamilika.
Hii
ni maktaba ya 24 kujengwa hapa nchini kwa ajili ya watoto wa shule za
msingi moja kati ya hizo ni maktaba ya watu wazima iliyopo ndani ya
Jengo la Makumbusho jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment